Mgonjwa wa dharura atibiwe kwanza, fedha baadaye

0
200

Serikali imewataka waganga wakuu wa vituo vyote vya kutolea huduma za afya kuhakikisha kuwa wagonjwa wote wanaopokelewa kwa dharura wanapatiwa kwanza huduma za afya ili kuokoa maisha yao, na taratibu nyingine zifuate baada ya kuwa wamehudumiwa.

Hayo yameelezwa na Naibu Waziri wa Afya, Dkt. Godwin Mollel wakati akijibu swali la Mbunge wa Moshi Mjini, Priscus Tarimo aliyetaka kujua kwanini watu waliopata ajali wanapokwenda kwenye vituo vya kutolea huduma za afya hulipa gharama za kumwona daktari na kugonga muhuri.

Amesema “Serikali kupitia Sera ya Afya ya Mwaka 2007 imeweka utaratibu wa wagonjwa wote wa dharura kupatiwa huduma za afya za dharura kwanza pasipo kikwazo cha kulipia hadi hapo changamoto za kiafya za dharura zitakapokwisha.”

Aidha, amesema kwa sasa hadhani kama kuna ulazima wa mtu aliyepata ajali kuhitaji fomu ya PF3 ili kupata matibabu, lakini wataendelea kufuatilia pamoja na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi waone namna ya kuliweka vizuri jambo hilo.

Katika hatua nyingine amesema Serikali imepanga kutumia shilingi Bilioni 30 kuimarisha huduma za watoto wachanga kwenye hospitali 100 nchini kwa kujenga wodi maalum (NCU) za watoto wachanga, watoto njiti na ununuzi na usambazaji wa vifaa tiba ikiwemo mashine za kuwasaidia watoto wachanga njiti kupumua.