Rais Magufuli: Watendaji wa Kata tangazeni utekelezaji wa miradi mikubwa

0
226

Rais John Magufuli amewataka Watendaji wa Kata nchini kutangaza mafanikio yaliyopatikana katika utekelezaji wa miradi mikubwa ya ujenzi wa barabara, maji, umeme, reli na hata vituo vya afya.

Akihutubia katika mkutano baina yake na Watendaji wa Kata zaidi ya Elfu Nne kutoka nchi nzima Ikulu jijini Dar es salaam, Rais Magufuli amewataka Watendaji hao kuyatangaza mafanikio ya utekelezaji wa miradi yote mikubwa inayotekelezwa katika kata zao na maeneo mengine.

Akitaja miradi ya barabara iliyotekelezwa na serikali hadi sasa ni pamoja na barabara ya kutoka Tunduma – Sumbawanga – Starike katika mkoa wa Rukwa, barabara ya Mpanda -Tabora yenye urefu wa Kilomita 350 na barabara ya Tabora – Uvinza – Kigoma inayounganisha mikoa ya Kigoma na Tabora.

Kuhusu miradi ya maji, Rais Magufuli amesema kuwa serikali inatekeleza mradi mkubwa wa maji katika jiji la Arusha ambapo zaidi ya Shilingi Bilioni 500 zinatumika katika mradi huo wenye uwezo wa kuhudumia Wakazi wa jiji hilo kwa zaidi ya mara mbili ya mahitaji halisi.

Rais Magufuli pia amezungumzia mradi wa kusambaza Umeme Vijijini ambapo amesema kuwa, ndani ya kipindi cha miaka mitatu serikali imesambaza umeme kutoka vijiji 2,000 mwaka 2016 hadi kufikia vijiji zaidi ya 7, 000 kwa hivi sasa.

Kuhusu huduma za Afya, Rais Magufuli amesema kuwa, lengo la serikali ni kuhakikisha inaboresha na kujenga vituo vya afya katika kila Kata na kukarabati vilivyopo ili kutoa huduma bora za afya kwa Wananchi.