Tanzania na Kenya wajadili namna ya kuimarisha mipaka

0
190

Mkuu wa mkoa wa Arusha, -Mrisho Gambo ametoa wito kwa Wajumbe wanaoshiriki kikao cha uimarishaji mipaka kati ya Tanzania na Kenya,  kutumia kikao hicho kutafuta ufumbuzi wa kudumu wa changamoto za mipaka badala ya kushindana.

Gambo ametoa wito huo jijini Arusha,  wakati wa akifungua kikao cha muendelezo wa uimarishaji mipaka ya Kimataifa baina ya Tanzania na Kenya.

Amesema kuwa, anafarijika kuona utatuzi wa changamoto za mipaka ya Kimataifa kati ya Kenya na Tanzania unafanywa na nchi husika bila kushirikisha mataifa ya nje na kwamba hali hiyo inaonyesha namna nchi hizo zinavyoweza  kukaa pamoja kwa kujiamini na kupata ufumbuzi wa masuala yake.

Amewataka Wajumbe hao kutafuta ufumbuzi wa changamoto za mipaka ya kimataifa kati yao kwa kukubaliana na kwa  kuzingatia  tamaduni za nchi hizo, pamoja na miongozo ya viongozi wa nchi husika.

Kwa upande wake Naibu Katibu Mkuu wa wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mathias Kabundugulu amesema kuwa, kikao hicho cha siku Tano ni muendelezo wa vikao vya uimarishaji mipaka ya Kimataifa katika maeneo mbalimbali ya mipakani, lengo likiwa ni kuondoa changamoto kama ilivyoelekezwa na Umoja wa Afrika (AU).

Kwa mujibu wa Kabundugulu, kikao hicho kitapokea taarifa ya ukaguzi wa kipande cha mpaka cha kilomita 128 kutoka eneo la ziwa Natron hadi Namanga mkoani Arusha,  ili kuimarisha mpaka huo hadi Tarakea mkoani Kilimanjaro na baadaye Jasini mkoani Tanga.