Serikali yaanza kujenga Daraja ili kurahisisha shughuli za Kiwanda cha Sukari Kagera

0
164
Mitambo ikiwa katika eneo ambalo litajengwa Daraja karibu na Mashamba ya Miwa ya kiwanda cha Sukari cha Kagera

Serikali imesema itaendelea kushirikiana na wawekezaji ili kuhakikisha kunakuwapo na mazingira mazuri ya kufanyia shughuli zao na kukuza biashara na uwekezaji kwa lengo la kuongeza tija katika ukuaji wa uchumi wa Taifa.

Katika hatua za kutekeleza maelekezo hayo, uongozi wa kampuni ya Kagera Sugar walitoa ombi kwa Serikali kuwajengea daraja kwenye mto Kagera ili waweze kufika kwa urahisi mashamba yao ambayo yapo upande wa pili wa mto Kagera.

Ombi la kujenga daraja hilo liliwasilishwa na kampuni hiyo kutokana na sababu kwamba ili kufikia mashamba yao yaliyopo upande wa pili wa mto wanapitia Wilaya ya Karagwe ambapo inawachukua umbali wa takribani km 140 kwenda na kurudi kila siku ikilinganishwa na endapo daraja litajengwa itawawezesha kufikia mashamba hayo katika umbali wa km 2-5.

Katika kuonesha kwamba kampuni ilikuwa na uhitaji wa daraja hilo, tayari ilikuwa imenunua baadhi ya vifaa kwa ajili ya ujenzi wa daraja hilo ambapo Mhe. Rais aliridhia na kuunga mkono jitihada hizo ambapo aliahidi kujenga daraja kwa kushirikiana na kampuni. Tayari ujenzi wa daraja umeanza na thamani ya ujenzi huo ni bilioni 29.5 za kitanzania ambapo Kagera Sugar walinunua daraja la sh. 4.5 bilioni na Serikali inalijenga daraja na kulisimika pamoja na kujenga barabara ya km 18 kwa jumla ya Tsh.25 billioni.

TIC kama mdau wa uwekezaji imefurahishwa na kupongeza hatua hiyo ya Serikali na kwamba itaendelea kusaidia miradi mingine yenye uhitaji kama huo kwa maslahi ya maendeleo ya nchi yetu.