Timu ya Taifa ya soka ya Tanzania, -Taifa Stars imewasili jijini Kampala nchini Uganda tayari kwa mchezo wao wa kufuzu kwa michuano ya Afrika dhidi ya timu ya Taifa ya nchi hiyo utakaochezwa siku ya Jumamosi Septemba Nane.
Msafara wa Taifa Stars una wachezaji 23 na makocha watatu wakiongozwa na kocha mkuu Emmanuel Amunike ambae mchezo dhidi ya Uganda utakuwa mchezo wake wa kwanza akiwa kocha wa timu hiyo.
Kikosi hicho cha Taifa Stars kina wachezaji tisa wanaocheza soka la kulipwa nje ya nchi wakiongozwa na nahodha Mbwana Samatta anaecheza soka kwenye timu ya Genk ya Ubelgiji.
Akizungumza kabla ya kuondoka nchini, kocha Amunike amesema kuwa wanaenda Uganda huku wakiwa na matarajio ya kurejea na matokeo chanya ili kuweza kuibua matumaini ya kufuzu kwa michuano ya Afcon.
“Tuna hakika tutapata matokeo chanya kwenye mchezo huo wa Jumamosi dhidi ya Uganda na huo ndio mpango wetu” amesema Amunike.
Pia kocha huyo amesema kuwa amefurahi kuweza kuwa na wachezaji wote wanaocheza soka nje ya nchi na wale wanaocheza soka hapa nchini.
“Tunaenda Uganda kusaka ushindi, hivyo tutajitahidi kushambulia na wakati huohuo kulinda lango letu ili tusiruhusu kufungwa” amesema kocha huyo Mnigeria.
Kwa upande wake nahodha Mbwana Samatta amesema kuwa mchezo huo utakuwa mgumu kwa sababu ni mchezo wa majirani, lakini wao wanenda kupambana ili kuibuka na ushindi.
“Kama nilivyosema huu ni mchezo wa majirani, hivyo lazima utakuwa mgumu na tunawajua wachezaji wa Uganda kwa sababu tumecheza nao mara nyingi na siku zote mchezo wetu dhidi yao unakuwa mgumu” amesema Samatta.
Pia Samatta amesema kuwa mipango yao sio kwa Uganda tu bali kwenye michezo yote ya kundi lao la L katika kufuzu kwa michuano ya Afrika ya mwaka 2019 itayofanyika huko nchini Cameroon.
Huu ni mchezo wa pili kwa Taifa Stars wa kufuzu kwa michuano hiyo ya Afcon baada ya kutoka sare ya bao moja kwa moja na Lesotho mwaka 2017 hapa nchini, hivyo Taifa Stars inatakiwa kushinda mchezo huo dhidi ya Uganda ili kuweza kuibua matumaini yao ya kufuzu kwa michuano hiyo ya Afcon.
Tanzania haijafuzu kwa muda mrefu michuano ya Afcon ambapo kwa mara ya kwanza na mwisho kufanya hivyo ilikuwa mwaka 1980 yaani miaka 38 iliyopita na sasa kocha Emmanuel Amunike ana kibarua kigumu cha kuipa mafanikio timu hiyo.