Makocha wa vilabu vikubwa Barani Ulaya wamelitaka Shirikisho la soka barani humo (UEFA) kuangalia uwezekano wa kupitia upya sheria ya bao la ugenini katika mashindano ya bara hilo.
Akizungumza baada ya kumalizika kwa mkutano wa UEFA ulioshirikisha makocha hao nchini Uswiss, Kaimu Katibu Mkuu wa shirikisho hilo Giorgio Marchetti amesema wao wanafikiri kuwa katika wakati huu kufunga bao ugenini imekuwa jambo rahisi tofauti na miaka iliyopita, hivyo sheria hiyo ni vema ifanyiwe mabadiliko.
Mkutano huo ambao ni wa mwaka umehudhuriwa na makocha wa vilabu vikubwa Barani Ulaya akiwemo kocha wa Manchester United, – Jose Mourinho, kocha wa Arsenal, – Unai Emery na mtangulizi wake Arsene Wenger, Massimiliano Allegri wa Juventus, Julen Lopetegui wa Real Madrid, kocha wa Napoli,- Carlo Ancelotti na Thomas Tuchel kutoka Paris St-Germain.
Sheria hiyo ya bao la ugenini kwa mara ya kwanza ilianzishwa mwaka 1965 kwenye michuano ya kombe la washindi Barani Ulaya kama njia mbadala ya kupata mshindi tofauti na urushaji wa shilingi au kutumia uwanja wa ugenini kwa timu zote mbili (neutral ground) ili kuepuka baadhi ya gharama ikiwemo usafiri.
Kaimu Katibu Mkuu huyo wa UEFA Giorgio Marchetti amesema kuwa makocha hao wa vilabu vikubwa Barani Ulaya wanaamini kuwa sheria ya bao la ugenini inadumaza soka kwa kuwa inahamasisha timu ngeni katika mchezo kushambulia muda wote huku wenyeji wakijilinda kuhofia kuruhusu bao la nyumbani na hivyo kupoteza ladha ya mchezo.