Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema serikali inatambua mchango unaotokana na matokeo ya tafiti zinazofanywa hapa nchini ikiwemo ugunduzi wa fuvu la binadamu ambao umeijengea sifa Tanzania ndani na nje ya nchi.
Waziri Mkuu ametoa kauli hiyo wakati akizungumza mara baada ya kuzindua makumbusho ya kisasa ya Dkt Mary Leakey na mnara wa kumbukumbu ya fuvu la binadamu wa kale ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya miaka 60 ya ugunduzi wa fuvu la binadamu ambapo amesisitiza umuhimu wa kuboresha hifadhi za mali kale.
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akizindua na kutembelea makumbusho ya kisasa ya Dkt Mary Leaky pamoja na kuona nyumba na vifaa alivyokuwa anavitumia wakati akifanya tafiti lakini pia amezindua mnara wa kumbukumbu ya fuvu la binadamu wa kale.
Waziri wa Maliasili na Utalii Dkt Hamisi Kigwangala amesema katika kuadhimisha miaka 60 ya ugunduzi wa fuvu la binadamu wa kale wizara itahakikisha inaendeleza tafiti zilizopo ili kuidhihirisha Dunia chimbuko la binadamu huku Waziri wa Habari,Utamaduni Sanaa na Michezo Dkt Harrison Mwakyembe amesema katika kulinda tamaduni watahakikisha wanakuwa wasimamizi bora.
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akazungumza katika hadhara ya wananchi waliofika katika eneo hilo,amesema anatambua mchango mkubwa unaofanywa na watafiti huku akiomba makumbusho yaboreshwe ili kulinda rasilimali zilizopo.
Kuhusu suala la changamoto baina ya wananchi na Mamlaka ya Ngorongoro,Waziri Mkuu amewataka wananchi kuwa na subira ili ufumbuzi uweze kupatikana.