Baraza la kijeshi la Sudan linaloongoza serikali ya Mpito ya nchi hiyo na viongozi wa upinzani, wametia saini makubaliano ya mgawanyo wa madaraka, baada ya mazungumzo yaliyofanyika usiku kucha, yaliyokua na lengo la kumaliza mgogoro wa kisiasa nchini humo.
Chini ya makubaliano hayo, serikali ya mpito ya Sudan, itashirikisha wajumbe kutoka pande zote mbili, ambao wataliongoza Taifa hilo kwa muda wa miaka mitatu mpaka utakapofanyika uchaguzi Mkuu.
Wachunguzi wa masuala ya kisiasa nchini Sudan wamesema kuwa, kusainiwa kwa makubaliano hayo ya mgawanyo wa madaraka, kutamaliza kabisa maandamano yaliyokua yakifanywa na raia wa nchi hiyo waliokua wanataka kurejeshwa kwa utawala wa kiraia.
Maandamano nchini Sudan yalianza mwezi Aprili mwaka huu, baada ya kuondolewa madarakani kwa Rais Omar El Bashir.