Tanzania yahitaji wawekezaji kutoka China

0
2714

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema kuwa Tanzania inahitaji wawekezaji wakubwa kutoka China ambao watawekeza kwenye viwanda vya mazao ya kilimo, samaki na mifugo.

Akizungumza jijini Beijing na Waziri wa Kilimo wa China,- Han Changfu, Waziri Mkuu Majaliwa amesema kuwa Tanzania imeamua kukuza uchumi wake kupitia sekta ya viwanda hivyo China ni nchi sahihi kushirikiana nayo kwa sababu ina wawekezaji wa kutosha wenye ujuzi mkubwa katika sekta hizo.

Aidha Waziri Mkuu Majaliwa amesema kuwa Tanzania inahitaji kupata soko la mbaazi na soya nchini China ili kuwawezesha wakulima kuwa na soko la uhakika la mazao hayo.

Kwa upande wake Waziri wa Kilimo wa China, Han Changfu amesema kuwa nchi yake iko tayari kutoa elimu na mafunzo kwa Watanzania hasa maafisa ili wafanye kazi zao kwa ufanisi zaidi.