Simba na Yanga zampigia debe Karia

0
115

Mwenyekiti wa klabu ya Simba SC, Murtaza Mangungu ameuomba Mkutano Mkuu wa mwaka wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) kumthibitisha Rais Wallace Karia kuendelea kuwa Rais wa Shirikisho hilo awamu ya tatu.

Mangungu ametoa mapendekezo hayo leo Desemba 21, 2024 katika mkutano huo unaofanyika mkoani Kilimanjaro ambapo hoja yake imeungwa mkono na wajumbe akiwepo Rais wa klabu ya Yanga SC, Mhandisi Hersi Said.

“Mafanikio makubwa ambayo Rais wa TFF pamoja na kamati tendaji ya TFF yamekuwa ni sababu kubwa ya maendeleo ya mpira wa miguu katika nchi yetu, sisi kama wana soka katika taifa hili tunajivunia sana uongozi wako Rais, tunajivunia utendaji wako, tunajivunia uchapa kazi wako lakini pia nafasi yako kama mlezi wa soka katika taifa letu nakupongeza sana” amesema Hersi

Akitolea ufafanuzi wa jambo hilo, Makamu wa kwanza wa Rais TFF, Athuman Nyamlani amesema haiwezekani kupitisha suala hilo katika mkutano huo ambao sio wa uchaguzi ambapo itakinzana na utawala bora wa taasisi hiyo na kuahidi kulifanyia kazi wakati ukifika.