MNH warejesha sauti ya mtoto aliyekatwa shingo na hausigeli

0
27

Sauti ya mtoto Maliki Hashimu (6), mkazi wa Goba, Jijini Dar es Salaam imerejea kwa asilimia 100 baada ya kukamilisha hatua zote za matibabu katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) kutokana na majeraha makubwa aliyopata yaliyotokana na kukatwa na ‘hausigeli’ na kitu chenye ncha kali shingoni, Julai mwaka huu.

Tukio hilo lilitenganisha njia ya hewa chini ya sanduku la sauti na kusababisha Maliki ashindwe kupumua na kuongea huku akiwa na maumivu makali licha ya kupoteza damu nyingi.

Akizungumza na waandishi wa habari kuhusu maendeleo ya kitabibu ya mtoto huyo, Mkurugenzi Mtendaji wa MNH, Prof. Mohamed Janabi amesema matibabu ya mtoto Maliki yamefanyika hatua kwa hatua na watalaamu wamejiridhisha kulingana na huduma alizopata mtoto huyo kwa kurejesha kila kilichokuwa kimepata hitilafu kwenye shingo yake na kwamba sasa yupo salama kuendelea na shule na maisha yake ya kawaida.

Naye Daktari Mbobezi wa Upasuaji Shingo na Mkuu wa Idara ya Pua, Koo na Maskio, Dkt. Aslam Nkya, amesema mtoto huyo alipofikishwa hospitalini alikua na jeraha mbele ya shingo, lililoharibu tezi la mbele liitwalo thyroid gland baada ya kukatwa katikati na kusababisha avuje damu kwa wingi, kupata maumivu makali sehemu iitwayo trachea ambako hewa inayotoka kwenye mapafu hupita ili iweze kwenda kwenye sanduku la sauti kumwezesha kuhema na kuongea. Lakini amesema vyote vimerejeshwa katika hali yake ya kawaida.

Mama mzazi wa mtoto huyo, Shani Charles, kipekee amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kulipa gharama za matibabu ya mtoto huyo kiasi cha shilingi milioni 15, watoa huduma wote wa MNH walioshiriki kumhudumia mpaka hatua aliyofikia leo kuruhusiwa kurudi nyumbani.

Shani pia amewashukuru Watanzania walioguswa na tukio hilo pamoja na vyombo vya habari vilivyofuatilia kwa karibu tukio hilo lililokaribia kupoteza uhai wa mwanawe au kumfanya asiwe mwenye uwezo wa kuongea tena.

✍️ @marikiadrina