Rais William Ruto amerusha ‘madongo’ dhidi ya aliyekuwa naibu wake, Rigathi Gachagua, ambaye aliondolewa ofisini kupitia mchakato wa kikatiba uliohusisha Bunge akidai alijikuta mpweke!
Akizungumza kwa hisia kali katika hafla ya kuapishwa kwa Naibu Rais mpya, Profesa Kithure Kindiki leo Novemba 1, 2024, Rais Ruto ameeleza alivyojikuta kama mtu wa “sauti ya upweke” ndani ya Serikali, akifafanua kwamba alikosa msaada wa kutosha kufikisha vizuri programu za utawala wake kwa wananchi.
Ruto amemsifu Kindiki kwa uwezo wake wa kiakili na ufasaha wa maneno, akisema, “Nahitaji sauti yako. Nahitaji akili yako kunisaidia mimi na mawaziri wetu kueleza na kuwasilisha kwa wananchi mambo tunayofanya.”
Rais amesisitiza kuwa katika kipindi cha miaka miwili iliyopita, alibaki kuwa msemaji pekee wa mipango ya serikali yake. “Nimekuwa natoa sauti ya upweke katika Serikali ninapotaka kuzungumzia programu zetu na kufafanua kazi tunazofanya.”
Katika ombi la moja kwa moja kwa Kindiki, Ruto ameonesha imani yake kwa uwezo wa naibu wake huyo mpya kukidhi nafasi ambayo anahisi haikutekelezwa vyema hapo awali aliposema, “Wewe ni mfasaha, ndugu yangu; wewe ni mwerevu, ndugu yangu. Nina imani kwamba utafanya kile ambacho nimekikosa kwa miaka miwili iliyopita. Najua utaweza.”
Hii ni mara ya kwanza kwa Rais Ruto kudokeza miongoni mwa mambo yaliyosababisha mfarakano na naibu wake, tangu mashambulizi ya kisiasa yaliyopelekea kuondolewa kwa Gachagua madarakani yalipoanza.