Ruto: Kwa nini nilimchagua Kindiki kuwa Naibu Rais

0
1324

Rais William Ruto wa Kenya ametoa sababu zilizomsukuma kumchagua Profesa Kithure Kindiki kuwa naibu wake, kufuatia wiki kadhaa za ukimya wakati wa mchakato wa kumwondoa Rigathi Gachagua madarakani.

Akizungumza wakati wa sherehe za kuapishwa kwa Kindiki katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Kenyatta (KICC), Rais Ruto amesema kuwa Kindiki ameonesha uadilifu na weledi wa hali ya juu katika nafasi zake alizoshika kama Waziri wa Mambo ya Ndani, Seneta wa zamani wa Tharaka Nithi na Kiongozi wa Wengi katika Seneti.

Ruto amebainisha kuwa ujuzi wa Kindiki katika uongozi utasaidia sana katika kusaidia utawala wake kutekeleza Ajenda ya Mageuzi ya Kiuchumi ya Chini Juu (BETA). “Ninaweza kuthibitisha kuwa katika nafasi zote hizi, ameonesha kujitolea kwa hali ya juu, ufanisi mkubwa, na weledi bora, huku akiendelea kutoa matokeo zaidi ya matarajio,” amesema Rais Ruto.

“Yeye ni msomi mwenye sifa za juu na mwenye umahiri wa kipekee, ambaye kazi yake imekuwa na mafanikio bora, yanayoonesha maono yake ya mabadiliko chanya na kujitolea kwake katika viwango vya juu vya ufanisi.”

Rais amekiri kuwa nafasi ya Naibu Rais inapaswa kuwaunganisha Wakenya wote na si kutumikia maslahi binafsi au kuwagawa. Wengi wametafsiri maneno haya ya Rais kama dongo kwa Gachagua ambaye amekuwa akilalamikiwa kwa kuangalia zaidi maslahi ya eneo la Mlima Kenya.

Chanzo: Citizen Digital