Maafisa wa Jeshi la Polisi nchini wametakiwa kujenga tabia ya kujikumbusha sheria mbalimbali zikiwemo zinazohusu masuala ya uchaguzi, ili kuepuka kuyumbishwa na wanasiasa wanaoamua kupotosha yaliyomo katika sheria hizo kwa maslahi binafsi.
Kauli hiyo imetolewa Jijini Dodoma na Mkurugenzi wa Uchaguzi wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi. (INEC) Kailima Ramadhani wakati akifungua mafunzo ya Wakuu wa Upelelezi wa wilaya nchini.
Amesema mafunzo ya aina hiyo ni muhimu kwa kipindi hiki ambacho kuna sheria mpya mbili zinazosimamia masuala ya uchaguzi.
“Katika sheria zote mbili yapo mabadiliko makubwa katika maeneo mbalimbali ambayo ni muhimu sana kwenu kuyafahamu kipindi hiki ambacho uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura unaendelea na mwakani itakuwa ni uchaguzi mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani,” amesema Kailima na kuongeza kuwa
“Uelewa wenu kuhusu sheria hizi utasaidia sana usimamiaji wa sheria na kuchukua hatua za udhibiti wa uvunjifu wa sheria hizo pamoja na sheria zingine ili watakaokiuka sheria hizo waweze kufunguliwa mashtaka ipasavyo na kuwatendea haki kwa kitakachoamuliwa na mahakama”.
Lengo la mafunzo hayo kwa maafisa hao wa Jeshi la Polisi nchini ni kuwajengea uelewa kuhusu haki za vyama, wananchi na makundi mengine katika vipindi vyote vya uchaguzi ambavyo ni kabla ya uchaguzi mkuu, wakati wa uchaguzi na baada ya uchaguzi.