Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) imesema kuwa uchaguzi wa rais na wabunge uliofanyika nchini Msumbiji Oktoba 9, 2024, kwa kiasi kikubwa ulizingatia kanuni na miongozo ya uchaguzi wa kidemokrasia kama SADC inavyosisitiza kwamba kuwe na haki, uhuru, usawa na uwazi.
Hayo ni kwa mujibu wa taarifa ya awali kuhusu uchaguzi huo iliyotolewa na Mkuu wa Misheni ya SADC ya Uangalizi wa Uchaguzi huo Mkuu wa Msumbiji, Amani Abeid Karume ambaye ni Rais Mstaafu wa Zanzibar.
Karume amesema katika kutekeleza jukumu lake, misheni hiyo iliangalia masuala mbalimbali muhimu kabla na wakati wa uchaguzi, ikiwemo hali ya siasa na usalama nchini humo, usimamizi wa uchaguzi, ripoti za vyombo vya habari kuhusu uchaguzi na uwakilishi wa jinsia, mambo ambayo yametekelezwa kwa kiasi kikubwa.
Aidha, amesema Misheni hiyo aliyoiongoza imeshuhudia nchi hiyo ikiwa katika hali ya amani na utulivu katika kipindi chote cha kabla na wakati wa uchaguzi, ambapo kampeni, mikutano ya hadhara na mchakato wa upigaji kura vilifanyika kwa amani, licha ya changamoto za kiusalama katika baadhi ya maeneo, hususan jimbo la Cabo Delgado.
Pia Dkt. Karume ametumia nafasi hiyo kuwashukuru wananchi wa Msumbiji kwa kuonesha ukomavu wa kisiasa na uvumilivu katika kipindi chote cha uchaguzi, akiwataka washindani wa kisiasa kufuata taratibu za kisheria endapo kutatokea migogoro yoyote kuhusu uchaguzi.
Pia ametoa wito kwa wadau mbalimbali kuendelea kuwa watulivu na wavumilivu wakati mamlaka za usimamizi wa uchaguzi zikikamilisha kujumlisha matokeo ya uchaguzi kabla ya kutangazwa rasmi, akiwaomba kuendelea kuhamasisha amani, uvumilivu na utulivu kupitia majukwaa mbalimbali katika kipindi hiki cha baada ya uchaguzi.
Kulingana na misingi na miongozo ya SADC inayosimamia uchaguzi wa kidemokrasia iliyorekebishwa mwaka 2021, misheni hiyo itatoa taarifa ya mwisho kuhusu uchaguzi huo siku 30 baada ya kutolewa kwa taarifa ya awali.
Misheni ya SADC, iliyozinduliwa rasmi Oktoba 3, 2024, ilipeleka waangalizi 52 katika majimbo yote 11 ya Msumbiji ili kuangalia uchaguzi huo.
Dkt. Karume aliteuliwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mwenyekiti wa Asasi ya Siasa, Ulinzi, na Usalama, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kuongoza misheni hiyo.