Vijana toeni maoni juu ya Tanzania muitakayo

0
301

Spika wa Bunge la Tanzania, Dkt. Tulia Ackson ambaye pia ni Rais wa Umoja wa Mabunge Duniani, amewataka vijana kuchangamkia fursa adhimu ya kutoa maoni kuhusu Tanzania waitakayo ili kuweza kuwa na mwafaka wa pamoja kama vijana kwa miaka 25 ijayo.

Dkt. Tulia ametoa wito huo akirejea takwimu za sensa ya watu na makazi ya mwaka 2022 iliyoonesha kuwa zaidi ya asilimia 77 ya Watanzania wote ni watoto na vijana na hivyo akasisitiza kwamba hatma ya Tanzania ipo mikononi mwao, hasa wale wa miaka 15-35 ambao ni asilimia 34.5 ya Watanzania wote.

“Lazima vijana mwone Dira hii ya Taifa ya Maendeleo kuwa ni ya kwenu na ni nafasi yenu ya kutoa maoni, kushauri na kuchangia ufanisi wa Dira ya Mwaka 2050. Hii Dira ni ya vijana,” amesema.

Dkt. Tulia ambaye ni mgeni rasmi kwenye kongamano la Kikanda, Kanda ya Kusini amesema hayo leo Jumamosi Agosti 03, 2024, kwenye Ukumbi wa Eden Highlands Jijini Mbeya ikiwa ni mwendelezo wa wizara yenye dhamana ya Mipango na Uwekezaji kukusanya maoni ya wananchi kama sehemu ya maandalizi ya uandishi wa Dira mpya ya Maendeleo ya Mwaka 2050.

Hata hivyo, Dkt. Tulia amesema watu wazima na wazee pia wana umuhimu mkubwa wa kutoa maoni yao katika dira hiyo kutokana na uzoefu na kufahamu mambo mengi ambayo yalifanyika kimakosa na yale ambayo hayakufanyika kiufanisi ili kusahihisha na kuyaweka mambo hayo katika namna nzuri ili yaweze kufanyiwa kazi.