Waziri Jafo atua kwa TBS

0
382

Waziri wa Viwanda na Biashara, Dkt. Selemani Jafo amelipongeza Shirika la Viwango Tanzania (TBS) kwa utendaji mzuri lakini akalitaka kuongeza nguvu katika utoaji wa huduma kwa wafanyabiashara hususani upatikanaji wa haraka wa nembo ya ubora wa bidhaa ili kukuza biashara, kuongeza ajira, pato la Taifa na uchumi kwa ujumla.

Ameyasema hayo leo mkoani Dar es Salaam wakati alipotembelea TBS kwa lengo la kujenga uelewa wa pamoja kuhusu shughuli mbalimbali zinazotekelezwa na shirika hilo ili kuongeza tija na ufanisi wa shirika katika kuwahudumia wafanyabiashara.

Aidha, ametoa wito kwa watumishi wa TBS kuendelea kufanya kazi kwa bidii, weledi na ushirikiano baina yao pamoja na kuepuka kuwa kikwazo katika utoaji huduma kwa wafanyabiashara ili kuiwezesha sekta binafsi kukua kwa kasi na kutimiza malengo ya Serikali ya Awamu ya Sita katika kujenga uchumi shindani wa viwanda.

Dkt. Jafo ameielekeza TBS kushirikiana vyema na Shirika la Kuhudumia Viwanda Vidogo (SIDO) pamoja na taasisi nyingine katika kuhakikisha wajasiriamali wengi wanapata nembo ya ubora na kufuatilia biashara zao ili kuhakikisha kiwango cha ubora wa bidhaa wanazozalisha haushuki kwa ajili ya kuwalinda walaji.