Madumu 1,731 ya mafuta yakamatwa yakisafirishwa kimagendo

0
279

Kikosi kazi cha Polisi Wanamaji Dar es Salaam kimekamata majahazi mawili katika Bahari ya Hindi, upande wa Dar es Salaam yakiwa na madumu 1,731 ya mafuta ya kupikia yenye ujazo wa lita 20 kila moja.

Majahazi hayo ni MV. Ukimaindi Poa na lingine halijafahamika jina wala namba zake za usajili. Yamekamatwa katika operesheni maalumu inayoendelea ya Kikosi Kazi cha Polisi Wanamaji yenye lengo la kudhibiti uhalifu Ukanda wa Bahari ya Hindi.

Watu wanne wanashikiliwa kufuatia tukio hilo wakidaiwa kuwa na nia ya kukwepa ushuru wa forodha.

Uchunguzi wa awali uliofanywa na Jeshi la Polisi umebaini kuwa watuhumiwa hao hawakuwa na nyaraka zinazothibitisha uhalali wa umiliki wa mafuta hayo ya kupikia pamoja na nyaraka za usafirishaji.

Katika hatua nyingine, Jeshi la Polisi Kikosi cha Wanamaji katika operesheni hiyo iliyoanza mwezi Mei, 2024 pia limekamata faiba boti nane ambazo hazina usajili wala majina, zikiwa zinajihusisha na usafirishaji wa abiria kwa njia hatarishi katika fukwe ya Kigamboni na Soko la Samaki Feri.