Jeshi lla Polisi nchini limepiga marufuku kampuni binafsi za ulinzi kutumia silaha aina ya Gobore kwa kazi za ulinzi, kwani ni kinyume cha sheria.
Badala yake limetaka wamiliki wa kampuni hizo kufuata utaratibu wa kisheria wa kumiliki silaha aina ya Shotgun, kwani ndizo zinazoruhusiwa kutumika kwa shughuli za ulinzi.
Kauli hiyo imetolewa na Msemaji wa Jeshi la Polisi nchini David Misime na kuongeza kuwa Jeshi la Polisi linatoa muda wa miezi mivili kuanzia Julai Mosi 2024 hadi Agosti 31, 2024 na baada ya kipindi hicho kutakuwa na msako mkali ambapo kampuni binafsi za ulinzi zitakazokutwa zikimiliki silaha hizo zitachukuliwa hatua za kisheria.
Jeshi la Polisi nchini limefikia hatua hiyo baada ya kubaini uwepo wa baadhi ya kampuni binafsi za ulinzi kumiliki silaha aina ya Gobore bila kuwa na vibali, kinyume na utaratibu unaozitaka kumiliki shotgun kwa ajili ya shughuli za ulinzi.