Bohari ya kuhifadhi gesi yazinduliwa Zanzibar

0
239

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt.Hussein Mwinyi ameipongeza kampuni ya Oryx Gas kwa kujenga bohari ya kwanza ya kuhifadhi nishati ya gesi, huku akizitaka kampuni za gesi kuhakikisha zinaweka mikakati itakayowezesha kupungua kwa bei ya gesi ili wananchi waipate kwa gharama nafuu.

Akizungumza mara baada ya kuzindua bohari hiyo ya kupokea na kuhifadhi gesi pamoja na miundombinu mingine jumuishi, Dkt. Mwinyi amepongeza ujenzi wa bohari hiyo na taasisi nyingine ambazo zimefanikisha ujenzi wa miundombinu jumuishi ya bandari ya Mangapwani ambayo itahusika na meli za mafuta na gesi pamoja na shughuli nyingine.

Amesema kuanzishwa kwa bohari ya kuhifadhi gesi Zanzibar kutaongeza chachu ya kuhamasisha matumizi ya nishati safi na hivyo kufikia malengo ya Rais Samia Suluhu Hassan kwamba ifikapo mwaka 2032 asilimia 80 ya wananchi watumie nishati safi ya kupikia.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Oryx Gas Tanzania Limited, Benoît Araman amesema kufunguliwa kwa bohari ya gesi Mangapwani, ni dhamira ya Oryx Energies ya kuwekeza katika miundombinu muhimu inayosaidia matumizi salama ya gesi ya LPG nchini.