Kuanza kwa safari za ndege za moja kwa moja za Shirika la Ndege la Zambia kutoka Zambia hadi Tanzania kutasaidia kuimarisha na kuharakisha ukuaji wa biashara kati mataifa hayo mawili pamoja na Ushoroba wa Kati.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Uchukuzi Profesa Godius Kahyarara amebainisha hayo mkoani Dar es Salaam baada ya kuzindua rasmi safari ya moja kwa moja ya ndege ya Shirika la Ndege la Zambia kutoka Lusaka mpaka Dar es Salaam.
Amesema katika nchi za Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) Zambia ni ya pili Kwa biashara na wafanyabishara wengi wa nchi hiyo wanaopitishia mizigo yao katika Bandari ya Dar es Salaam, hivyo wamerahisishiwa usafiri.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA) Musa Mbura amesema kuanza kwa safari hiyo inaifanya Tanzania kuwa na miruko ya moja kwa moja ya kimataifa 22 kutoka Uwanja wa Ndege Kimataifa wa Julius Nyerere.
Shirika hilo la ndege la Zambia litafanya safari mara tatu kwa wiki huku Shirika la Ndege la Tanzania (ATCL) likifanya safari za moja kwa moja kutoka Dar es Salaam hadi Lusaka mara tano kwa wiki.