Nape aipongeza TBC kwa kutoa elimu ya Bajeti

0
239

Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye amelipongeza Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) kwa kazi kubwa iliyofanya ya kuhabarisha umma kuhusu mchakato wa bajeti ili kila mwananchi aweze kuelewa.

“Niwapongeze TBC safari hii mmefanya kazi kubwa sana ya kufanya uchambuzi wa mambo kwenye bajeti. Bajeti inapaswa kuwa ni jambo la Watanzania kwa sababu itakwenda kutekelezwa na wao, itagusa maisha yao; Serikali na Bunge wanafanya kwa niaba ya wananchi, kwa hiyo ni vizuri wananchi wakaielewa,” ameeleza Waziri Nape.

Amesema hayo katika mahojiano maalum na Jambo Tanzania ya TBC1 yaliyohusu Bajeti Kuu ya Serikali kwa mwaka 2024/25 ambapo amesema “uchambuzi wa TBC umekuwa mzuri sana kwa kueleza baadhi ya michakato. Watu wengi walikuwa hawaijui michakato kwamba bajeti inatengenezwaje, maana yake nini, itafanyaje.”

Aidha, amesema baada ya Serikali kupitisha bajeti, wao kama wizara watazipa nafasi kila wizara kukutana na waandishi wa habari na kueleza kwenye mchakato wa bajeti ni kitu gani wamekipata.

“Kama wizara tutajipanga kupitia Idara ya Habari-Maelezo kuhakikisha tunawapa fursa Watanzania kusikiliza wizara moja moja imepata nini kwenye mchakato,” ameeleza waziri akisisitiza kuwa hilo ni muhimu kwani utekelezaji wa bajeti utahusisha watu ikiwemo kulipa kodi na miradi mbalimbali ya maendeleo na kijamii.

Aidha, amesema kuna umuhimu wa waandishi wa habari kuifahamu michakato ya uendeshaji wa shughuli za Bunge ili kuripoti kwa usahihi na kuepusha kuzua taharuki kwa wananchi kwa kueleza mambo ambayo si sahihi

“Tumeshauriana na Bunge kama mnataka shughuli zenu ziripotiwe vizuri tutengeneza utaratibu wa kuwafunza watu wajue,” ameeleza Waziri na kuongeza kuwa “kama wizara tuta-push [shinikiza] hili tupate waandishi, kwanza wa specialize shughuli za ripoti za Bunge, kila siku akija mpya atapotea tu.”

Amesema kuwa wizara itaweka mkazo kwa waandishi wa habari kuwa wabobezi kwenye maeneo husika kama vile uchumi, sheria, afya na maeneo mengine na ndio sababu ya kuanzishwa kwa Bodi ya Ithibati ambayo ni kuwawezesha waandishi kuwa wabobezi.