Tanzania yavuka lengo kupunguza vifo vya uzazi

0
193

Tanzania imevuka lengo la kupunguza vifo vya Mama na Mtoto ambapo kitaifa vifo vimepungua kutoka 556 mwaka 2016 hadi vifo 104 mwaka 2023 ambapo kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO) ilitegemewa vifo vipungue kufikia 225 ifikapo mwaka 2025.

Hayo yameelezwa bungeni jijini Dodoma na Naibu Waziri wa Afya Dkt. Godwin Mollel wakati akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalum, Restituta Mbogo aliyetaka kujua mikakati ya Serikali katika kupunguza vifo hivyo katika mkoa wa Katavi.

Dkt. Mollel amesema kuwa kwa takwimu hizo Serikali imefanikiwa kupunguza kabla ya muda uliotegemewa na kuvunja rekodi ya kufikia 104 badala ya 225 iliyotegemewa.

Ameongeza kuwa tangu mwaka 2020 hadi mwaka 2024 mtiririko wa vifo vya akina mama mkoani Katavi ni kama ifuatavyo: Mwaka 2020 vifo 56, mwaka 2021 vifo 41, mwaka 2022 vifo 36, mwaka 2023 vifo 33, na mwaka 2024 kuanzia Januari hadi Mei kuna vifo 15, hivyo kwa mujibu wa takwimu hizo kuna kupungua kwa vifo vitokanavyo na sababu za uzazi.