Sukari, gesi, kikokotoo moto bungeni

0
808

Kwa siku nne zilizopita, wabunge wamekuwa wakijadili Bajeti ya Serikali na Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa mwaka 2024/25 ambapo hoja zinazohusu sukari, gesi ya magari, kikokotoo, ubadhirifu au kubana matumizi ya fedha za umma pamoja na adhabu kwa mfanyabiashara kutokutoa risiti zimeonekana kuwagusa zaidi wawakilishi hao wa wananchi.

SUKARI

Kuhusu sukari, serikali inapendekeza kufanya marekebisho kwenye Sheria ya Sukari, Namba 6 ambapo pamoja na mambo mengine inalenga kuuwezesha Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) kununua, kuratibu na kuhifadhi pengo la sukari kwenye hifadhi ya chakula ya Taifa. Lengo la hatua hiyo ni kuwezesha upatikanaji wa sukari nchini na kuondoa uhodhi kwa baadhi ya wenye viwanda bila kuathiri dhamira ya serikali ya kulinda viwanda vya ndani.

Kumekuwa na maoni mchanganyiko kutoka kwa wabunge waliochangia eneo hili lakini wengi wao wameunga mkono mpango huo ili kulinda mwananchi. Mbunge wa Tandahimba, Katani Katani alisema “leo hii nitashangaa kuona mbunge ambaye atapinga kuletwa sheria hii bungeni, ili wananchi wetu waendelee kupata shida kila mwaka ya kupanda kwa bei ya sukari,” huku Mbunge wa Makete, Festo Sanga akisema mabadiliko ya sheria ya sukari yatasaidia kuondoa tabia iliyojengeka kwa wale waliopewa dhamana kufanya mambo kwa maslahi yao binafsi.

GESI

Kuhusu tozo ya shilingi 382 kwenye kila kilo moja ya gesi inayotumika kwenye magari, wabunge wengi wamepinga pendekezo hili ambapo Mbunge wa Geita Vijijini, Joseph Musukuma amesema ongezeko hilo litakwamisha lengo la kutaka kuwe na matumizi makubwa ya nishati salama ya gesi ambayo ni kipaumbele cha Rais Samia Suluhu.

Kwa upande wake Mbunge wa Muleba Kaskazini, Charles Mwijage alisema “tumekosea, na Mheshimiwa Waziri Mwigulu unisikilize, kwa nini unaweka ongezeko la pesa kwenye gesi, kwa nini gesi na watu wengi hawataki kuzungumza. Sisi gesi kwetu ni kinga, ni usalama kwamba endapo kuna tatizo kwenye ugavi sisi nchi tutabaki salama.”

Wabunge wameona pia kuweka kodi kutapunguza hamasa ya wenye magari kuhamia kwenye nishati hiyo ambayo pia ni rafiki wa mazingira.

KIKOKOTOO

Wabunge wa Viti Maalum, Halima Mdee na Esther Bulaya wamesema kuwa suala la serikali kuongeza malipo ya mkupuo ya pensheni hadi asilimia 40 ni danganya toto, badala yake wameitaka serikali kama kweli ina dhamira ya kuboresha maslahi ya watumishi warejeshe bungeni sheria hiyo ifanyiwe maboresho, pamoja na kanuni zake ili kuwanufaisha watumishi.

“Sote tunajua kikokotoo bado ni janga na hii haijaisha mpaka iishe. Hitaji lao lilikuwa asilimia 50 wachukue mafao kwa mkupuo,” amesema Bulaya.

WIZI WA FEDHA

Mbunge wa Gairo, Ahmed Shabiby yeye amelia na wizi wa fedha za umma akisema kwamba wezi hao wamejificha kwenye kivuli cha kusema ‘Mama Anaupiga Mwingi’ wakati wao ndio wanaoupiga kwa kuiba. “Nchi imefikia wakati sasa hivi, lazima tuseme ukweli, wapigaji wamekuwa wengi. Wengine utasikia tu, ‘Mama Anaupiga Mwingi,’ sio kwamba anaupiga mwingi anamsifia kwenye moyo, anaupiga mwingi yeye anaiba hela,” ameeleza.

Katika hatua nyingine amehoji Serikali kushindwa kutekeleza ahadi yake ya kukopesha magari kwa watumishi wa umma wanaostahili kupewa magari, badala ya Serikali kubeba mzigo wa kuwanunulia ni kugharamia magari kama njia ya kupunguza matumizi ya Serikali.

Wabunge pia wamehoji ununuzi wa mashangingi, hususani kwenye halmashauri huku nyingi bado zikitegemea ruzuku kutoka serikali kuu kujiendesha.

SHERIA YA KODI

Mbunge wa Kahama, Jumanne Kishimba amepinga mpango wa serikali wa kurekebisha Kifungu cha 86(1) cha Sheria ya Usimamizi wa Kodi kwa kuweka ukomo wa faini ya juu ya kosa la kutokutoa risiti wa kiasi cha shilingi 15,000,000. Amesema anayeuza bidhaa sio tajiri bali ni mfanyakazi, hivyo amehoji kwa nini mfanyakazi afanye kosa halafu adhabu apewe tajiri ambaye hafahamu kilichotokea. Pia, amependekeza mtu ambaye atanunua bidhaa au kulipia huduma na asipodai risiti naye apewe adhabu.

Wabunge wataendelea kuchangia hoja za serikali hadi Juni 26 mwaka huu, kisha watapiga kura kupitisha au kukataa bajeti hiyo.