Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ameielekeza Ofisi ya Taifa ya Mashtaka, mara upelelezi utakapokamilika, kuwafikisha mahakamani mara moja watuhumiwa wote waliohusika na mauaji ya mtoto Asiimwe Novath aliyekuwa na umri wa miaka miwili na nusu mkoani Kagera, ili iwe fundisho kwa watu wengine wanaofikiria kufanya vitendo kama hivyo.
Waziri Mkuu ametoa maelekezo hayo bungeni jijini Dodoma leo asubuhi alipokuwa akiwasilisha tamko la Serikali kuhusu ulinzi wa mtoto ambapo amewataka wananchi kuachana na imani potofu au mizaha inayolenga kuaminisha kuwa viungo vya watu wenye Ualbino vinaweza kuwaletea utajiri.
“Mizaha kama hii si tu inaonesha ukosefu wa heshima kwa watu wenye Ualbino na familia zao, lakini pia inachochea ubaguzi na unyanyapaa,” amesema huku akiwasihi wananchi wote kuheshimu haki za binadamu na kuepuka vitendo au lugha ambazo zinaweza kudhalilisha au kuumiza wengine.
Taarifa ya Serikali imeeleza kuwa Mei 30, 2024 mtoto Asiimwe, mkazi wa Kitongoji cha Mbale, Kijiji cha Mulamula, Wilaya ya Muleba, Mkoa wa Kagera alitekwa na vijana wawili saa 2:15 usiku akiwa nyumbani kwao Kebyera na mama yake.
Mmoja wa vijana hao alimkaba koo mama yake ambaye alikuwa nje ya nyumba na mwingine aliingia kwa haraka ndani na kumchukua mtoto na kutokomea naye kusikojulikana.
Juni 17 mwaka huu mwili wake ulipatikana ukiwa kwenye mfuko wa plastiki pembezoni mwa barabara itokayo Kijiji cha Ruhanga kwenda Kijiji cha Malele, Kata ya Ruhanga, ambapo baadhi ya viungo vya mwili wake vilikuwa vimeondolewa.
Ameeleza kuwa uchunguzi ulianza mara moja na unaendelea na hadi sasa washukiwa tisa wamekamatwa na Jeshi la Polisi.
Pia, wataalam wa Ustawi wa Jamii wanaendelea kutoa huduma ya msaada wa kisaikolojia kwa waathirika kupitia Maafisa Ustawi wa Jamii katika ngazi ya Mkoa wa Kagera na Halmashauri ya Wilaya ya Muleba.
Aidha, Waziri Mkuu amesema tukio hilo linaelekea kufanana na tukio lililotokea Mei 4 mwaka huu ambapo mtoto Julius Kazungu (10) mwenye Ualbino, mkazi wa Katoro, Geita, alivamiwa majira ya saa 2:00 usiku na mtu asiyejulikana ambaye alikuwa ameficha sura yake na kuanza kumkata na panga kichwani na mikononi. Mtoto huyo alilazwa na sasa anaendelea vizuri na Serikali ya mkoa inagharamia matibabu yake.