Mbunge wa Viti Maalum, Khadija Shaaban Taya (Keisha) mapema leo asubuhi alitoa hoja akilitaka Bunge kuahirisha shughuli zake ili kutoa nafasi kwa wabunge kujadili vitendo vinavyoendelea nchini kwa watu wenye Ualbino kushambuliwa ikiwemo kukatwa viungo vyao, hasa wakati uchaguzi unapokaribia.
Keisha amesema kuwa Mei 4 mwaka huu mkoani Geita mtoto anayeitwa Julius Kazungu (10) alijeruhiwa na kitu chenye ncha kali kichwani na mikononi.
Aidha, amesema Mei 30 mwaka huu mtoto Asimwe Novas aliibwa na watu wasiojulikana waliovamia nyumbani kwao, na alipatikana akiwa amefariki dunia Juni 17, 2024 huku baadhi ya viungo vya mwili wake vikiwa vimekatwa.
“Watu wenye ualbino hawana amani, hawana raha; wanaamini kwamba karibia na uchaguzi maisha yao yanakuwa hatarini,” amesema mbunge huyo akitokwa machozi huku akiomba wabunge wenzake kumuunga mkono ili Bunge lijadili hoja hiyo ikizingatiwa kuwa nchi inakwenda kwenye kipindi cha uchaguzi.
“Mheshimiwa Naibu Spika, naomba Bunge lako liahirishe shughuli zake, tujadili namna gani nzuri ya kuwalinda watu wenye Ualbino pamoja na watoto wetu, lakini pia tuitake Serikali ilete sheria kali ambazo zitaweza kuonesha mfano kwa watu wengine kutokufanya vitendo hivi,” ameeleza.
Hata hivyo, Naibu Spika Mussa Zungu alimwelekeza kuonana na Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi ili amweleze vizuri na apate majibu ya Serikali kwa usahihi.