Mpango ashiriki mazishi ya kitaifa Malaw

0
354

Makamu wa Rais Dkt. Philip Mpango amemwakilisha Rais Samia Suluhu Hassan katika mazishi ya Kitaifa ya Makamu wa Rais wa Malawi Dkt. Saulos Chilima aliyefariki dunia katika ajali ya ndege.

Ibada ya mazishi hayo imefanyika katika Uwanja wa Taifa wa Bingu uliopo Lilongwe nchini Malawi.

Akitoa salamu za rambirambi Dkt. mpango amesema Tanzania inatoa pole na kuungana na waombolezaji wote walioguswa na msiba huo katika kipindi hiki kigumu.

Amesema Hayati Chilima alikuwa kiongozi imara, mwanamajumui wa kweli wa Afrika ambaye wakati wote alitanguliza mbele maslahi ya wananchi anaowaongoza na Afrika kwa ujumla.

Pia amemtaja Hayati Chilima kama kiongozi aliyesimamia umoja, amani na usalama, mageuzi ya kiuchumi ya Malawi na utawala wa kidemokrasia nchini Malawi.

Makamu wa Rais amesema wananchi wa Malawi na Ukanda wote kwa ujumla wanapaswa kumuenzi Hayati Chilima kwa kuendeleza yale aliyosimamia na kuendelea kumuombea apumzike kwa amani.