Deni la Serikali lafikia Trilioni 91

0
185

Hadi Machi 2024, deni la Serikali lilikuwa shilingi Trilioni 91.7 ikilinganishwa na shilingi Trilioni 77 katika kipindi
kama hicho mwaka 2023, sawa na ongezeko la asilimia 19.1.

Hayo yameelezwa bungeni jijini Dodoma na Waziri wa Mipango na Uwekezaji Profesa Kitila Mkumbo wakati akiwasilisha Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa mwaka 2024/25 kuelekea kusomwa kwa bajeti kuu ya Serikali kwa mwaka ujao wa fedha.

Amesema kati ya kiasi hicho, deni la ndani lilikuwa shilingi Trilioni 30.7 na deni la nje lilikuwa shilingi Trilioni 60.9 na kwamba ongezeko la deni lilitokana na Serikali kuendelea kupokea fedha za mikopo ya zamani na mipya kwa ajili ya kugharamia miradi ya maendeleo, ikiwemo ujenzi wa miundombinu ya barabara, reli, viwanja vya ndege, umeme na maji.

Aidha, amesema ongezeko la deni lilichangiwa na kupanda kwa viwango vya kubadilisha fedha pamoja na kuongezeka kwa riba kwenye mikopo ya nje ambayo riba zake hutegemea mabadiliko ya hali ya soko (floating rates).