By: Erick Minja
Mratibu Kitaifa wa mradi wa Kuimarisha Ubora wa Elimu ya Sekondari (SEQUIP) Dkt. Meigaru Mollel
amewataka walimu wa TEHAMA kuwasaidia walimu wengine kufahamu umuhimu wa teknolojia ya habari na mawasiliano katika kukabiliana na mabadiliko mbalimbali.
Dkt. Mollel ameyasema hayo mkoani Mwanza wakati wa mafunzo ya teknolojia ya habari na mawasiliano yanayotolewa kupitia mradi wa SEQUIP, yanayoendelea katika Chuo cha Ualimu Butimba ambapo kundi la kwanza la walimu 600 kutoka mikoa ya Singida, Geita na Mara linapatiwa mafunzo hayo.
Amesema endapo walimu wengi zaidi watakuwa na ufahamu kuhusu TEHAMA wataweza kuwafundisha wanafunzi wao na hivyo kuwafanya kuitumia na kufanya vizuri darasani.
Aidha, Dkt. Mollel amesema Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia itajenga shule 1,000 ikiwa ni shule mbili kwa kila wilaya nchini, lengo likiwa ni kuboresha utoaji wa elimu hasa ya TEHAMA.