Ni vigumu bajeti ya serikali kukataliwa

0
197

Aliyewahi kuwa Mwenyeketi wa Kamati ya Bunge ya Bajeti, Omary Kigua amesema ni vigumu Kamati ya Bajeti kuikataa bajeti ya Serikali inayowasilishwa bungeni kwa sababu mchakato wa uandaaji wake ni shirikishi tangu mwanzo.

Kigua ambaye pia ni Mbunge wa Kilindi amesema hayo leo jijini Dodoma katika mahojiano maalum na Jambo Tanzania ya TBC1 na kuongeza kuwa mchakato huanza Novemba kwa Serikali kuwasilisha bungeni mapendekezo ya mpango wa bajeti kwa mwaka unaofuata ambapo kamati hupata nafasi ya kuishauri Serikali.

“Kabla ya bajeti ambayo inasomwa kesho, unakuwa ni mchakato wa muda mrefu sana, mchakato ambao unakuwa ni shirikishi,” amesema hayo akiongeza kuwa “kamati ya bajeti inayo nguvu sana na inayo uwezo wa kuishauri na kuisimamia Serikali.”

Ameongeza kuwa mpango huo huwasilishwa bungeni Februari na kusomwa na Wizara ya Fedha na kamati inawasilisha mapendekezo ya mpango huo, na wabunge hupata nafasi ya kuujadili, na maoni yao hujumishwa kwenye bajeti ya Serikali.

Aidha, wiki moja kabla ya bajeti ya Serikali kuwasilishwa, wajumbe wa kamati nyingine za bunge wanakuwa wajumbe wa kamati ya bajeti ambapo hukutana na Serikali kujadili yaliyotokana na wizara za kisekta, na Serikali inakuwa na nafasi nzuri ya kutoa majibu.

“Hadi inafika bajeti kuu ya Serikali inasomwa, kiujumla mambo yanakuwa yamekwenda vizuri kwa sababu inakuwa ni kazi shirikishi,” ameeleza Kigua.