Balozi wa Tanzania awasilisha nyaraka kwa Papa

0
324

Balozi Hassani Mwamweta amewasilisha Hati za Utambulisho kwa Kiongozi wa Kanisa Katoliki Duniani Baba Mtakatifu Francis nchini Vatican.

Hafla ya kuwasilisha hati hizo imehudhuriwa na viongozi waandamizi wa Vatican akiwemo Mwadhama Pietro Kadinali Parolin mwenye wadhifa wa Waziri Mkuu pamoja na Askofu Mkuu Paul Gallagher ambaye ni Waziri wa Mambo ya Nje wa Vatican.

Hatua hiyo ya Balozi Mwamweta kuwasilisha hati zake za utambulisho kwa Baba Mtakatifu Francis inampa uhalali Balozi huyo mwenye makazi yake Berlin, Ujerumani kutekeleza majukumu yake kama Balozi wa Tanzania kwenye Ukulu Mtakatifu ( Holy See).

Hiyo ni miongoni mwa mafanikio ya ziara ya kikazi ya Rais Samia Suluhu Hassan nchini Vatican Februari 11 hadi13, 2024, iliyolenga kudumisha ushirikiano wa kihistoria baina ya Tanzania na Vatican.

Mbali na Ujerumani na Vatican, Balozi Mwamweta pia anaiwakilisha Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwenye mataifa mengine sita ambayo ni Poland, Uswisi, Hungary, Jamhuri ya Czech, Bulgaria, Slovakia na Romania.