Serikali kuufumua mfumo wa uzalishaji na usambazaji sukari

0
185

Serikali imesema kuwa inakusudia kubadili mfumo wa uzalishaji na usambazaji wa sukari nchini ili kuhakikisha kuwa hali ya upungufu wa sukari, iliyopelekea bidhaa hiyo kupanda bei na kusababisha usumbufu kwa wananchi Desemba mwaka jana hadi Februari mwaka huu haijirudii tena.

Hayo yameelezwa bungeni jijini Dodoma na Waziri wa Kilimo Hussein Bashe wakati akichangia bajeti ya Wizara ya Fedha kwa mwaka 2024/25 ambapo amewahakikishia wananchi kuwa hatokubali kuona hali kama hiyo ikijirudia tena.

“Mfumo wa uzalishaji na usambazaji wa sukari tutau-confront [kabili] kuondoa mfumo wa cartel [genge] na kila mkoa utakuwa na msambazaji na kila kiwanda kitakuwa hakijiamulii bei kinavyotaka, Serikali itasimamia jambo hili bila matatizo yoyote,” Bashe ameliambia bunge.

Amesema kuwa mfumo wa sasa wa usambazaji sukari ni wa genge akitolea mfano msambazaji mmoja aliyeko mkoani Mwanza ambaye anahudumia mikoa 11, jambo ambalo amesema halikubaliki, na amewataka wahusika wakae mezani waone namna ya kusonga mbele.

Waziri Bashe amekosoa viwanda vya uzalishaji sukari nchini akisema kwamba mwaka jana waliwapa vibali kwa ajili ya kuingiza sukari tani 50,000 ili kukabili upungufu wa mwaka huu, lakini kampuni na wazalishaji hao hawakuwa wameingiza hata kilo moja kwa Desemba na Januari mwaka huu.

Ameeleza kuwa mwishoni mwa Januari waliingiza tani 250 licha ya kujua upungufu wa sukari ulikuwa mkubwa, na hata walipoingiza waliifungia kwenye bohari zao, hadi ikapelekea Serikali kuzifuata huko na polisi.

Amesema kutokana na kitendo hicho cha kutoingiza sukari, iliilazimu Serikali kutoa kibali kwa Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) kuingiza nchini sukari tani 410,000.

Aidha, Waziri Bashe amesisitiza kuwa Serikali italinda walaji, wakulima, viwanda na wafanyabiashara ili kuhakikisha upatikanaji wa bidhaa hiyo unakuwa shwari.