Mei 31 na Juni 03, 2024 Bunge limejadili bajeti ya Wizara ya Maliasili na Utalii kwa mwaka 2024/2025, ambapo wizara imewasilisha makadirio ya mapato na matumizi ya TZS Bilioni 348.
Kati ya fedha hizo shilingi Bilioni 250.9 ni kwa ajili ya matumizi ya kawaida na shilingi Bilioni 97.2 ni za miradi ya maendeleo.
Baada ya kuwasilishwa kwa bajeti hiyo, wabunge walipata wasaa wa kuchangia ambapo moja ya mambo yaliyoibua mjadala mkubwa ilikuwa ni athari za kibinadamu na mali zinazosababishwa na wanyama pori, hasa kwa jamii zinazoishi pembezoni mwa hifadhi na mapori mbalimbali, huku wakiitaka Serikali kueleza hatua ambazo imepanga kuchukua kudhibiti hali hiyo.
Kabla ya bajeti hiyo kuwasilishwa bungeni, Mbunge wa Buchosa, Erick Shigogo aliomba mwongozo wa Spika wa Bunge akitaka Bunge kusitisha shughuli zake za kila siku na kujadili jambo la dharura ambalo amesema kwa miaka mitatu iliyopita wananchi 36 katika jimbo lake wameliwa na mamba.
Akichagia hotuba hiyo ya bajeti Mbunge wa Viti Maalum, Martha Gwau ameonesha kutoridhiwa na majibu ya Serikali kuwa baadhi ya watu wamejenga kwenye njia za tembo, huku akisema kuwa mipaka iliyowekwa miaka ya nyuma lazima izingatie ongezeko la watu la sasa.
“Kwani nchi za wenzetu hawana hizi hifadhi? Kama wanazo, wao wamedhibiti vipi na sisi tunashindwa? Tunapomfanya mwananchi anakuwa na uoga, huwezi kuamka asubuhi kwenda shambani, au kufanya mambo giza likiingia […] watu wanahofu,” ameeleza.
Kwa upande wake Mbunge wa Viti Maalum, Hawa Mwaifunga amehoji upi ni mkakati wa wizara kudhibiti wanyama pori kuingia kwenye makazi ya wananchi, kwani kwenye bajeti iliyowasilishwa hatua iliyoelezwa ni ile inayohusu kudhibiti wanyama wanaoingia kwenye makazi.
“Tunataka watuambie mkakati wao kabla [wanyama] hawajaenda kukutana na hayo mabomu baridi [ambayo yanatumika kudhibiti tembo kwenye makazi ya watu], ili tuweze kujua na kunusuru wananchi wetu na mazao yao na wanyama hao hatari,” amehoji Mwaifunga.
Baada ya kuona hatua za kudhibiti wanyama zilizofanyika kwenye maeneo mengine, Mbunge wa Namtumbo, Vita Kawawa yeye amesema “tunaomba sasa [wizara] mfike na Namtumbo kwa sababu Namtumbo ni waathirika wakubwa sana wa tembo […] Tumeshapoeza wananchi watatu kwa hiyo tunaomba sana na zoezi lile na vifuta jasho vifike na kwetu.”
Mbunge wa Viti Maalum, Mariamu Kisangi amesema hatari inayotokana na wanyama mkoani Lindi inasababisha ugumu kwa wananchi kupata huduma za kijamii ikiwemo watoto kushindwa kwenda shule. Amesema kuwa bomu baridi linalotumika kufukuza tembo ni suluhisho la muda mfupi, na kwamba wanapofukuzwa eneo moja wanakwenda eneo jingine.
“Nawaomba wizara waendelee kufanya utafiti ili tupate suluhisho la kudumu. Wanapokwenda kule mbugani, kuna nini kinachowafanya wale tembo warudi tena kwenye makazi ya watu?” amehoji Kisangi akiongeza kwamba maeneo ya Liwale hawajaingilia maeneo ya hifadhi lakini bado wanyama wanakwenda kwenye makazi ya watu.
Wizara ya Maliasili na Utalii imeeleza kuwa mwaka 2024/2025 kupitia taasisi zake itaongeza ajira kwa askari 850 ili kuimarisha shughuli za uhifadhi na doria za kudhibiti matukio ya wanyama pori wakali na waharibifu.