Ekari 81 za bangi zateketezwa

0
156

Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA), Kanda ya Kaskazini kwa kushirikiana na vyombo vya ulinzi na usalama wilayani Arumeru, Hifadhi ya Taifa ya Arusha (ANAPA) pamoja na Serikali ya Kijiji cha Engutoto imefanikiwa kuteketeza ekari 81 za mashamba ya bangi zikiwa zimechanganywa na mazao ya nafaka.

Akizungumzia zoezi hilo, Ofisa Sheria wa DCEA Kanda ya Kaskazini, Benson Mwaitenda, amesema mamlaka pia imeteketeza magunia 20 ya bangi kavu pamoja na kufanikiwa kukamata watuhumiwa wanne katika operesheni hiyo.

Wakati wa zoezi la uteketezaji wa magunia hayo ya bangi, Mwaitenda ameitaka jamii kuacha kujihusisha na kilimo hicho cha bangi pamoja na matumizi ya dawa nyingine za kulevya kutokana na madhara yake kwa afya ya akili. Amesisitiza kwamba hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi yao pindi watakapojulikana.

Akitoa maoni yake kuhusu operesheni hiyo, mwanahabari Adrina Mariki ambaye yuko Arusha kikazi ameandika: “Yaani ukiwa huku Arusha ndio unaelewa kwa nini ni muhimu Serikali ipambane na hizi bangi. Aisee yaani vijana wengi akili zao zimetangulia, ukiwatazama tu unaona hii sura siyo.”