Wakazi 12 wa Ifakara mkoani Morogoro wamefikishwa katika mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu iliyopo mkoani Dar es Salaam, wakikabiliwa na mashtaka ya kuongoza genge la uhalifu na kujipatia shilingi Millioni 10 kwa njia ya udanganyifu.
Wakiwa mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu wa mahakama hiyo Ushindi Swalo, Wakili wa Serikali Tumaini Mafuru amedai watuhumiwa hao wanakabiliwa na mashtaka 32.
Mashtaka hayo ni pamoja na kuongoza genge la uhalifu walioufanya Januari Mosi hadi Mei 5, 2024, ambapo walituma jumbe fupi kwa watu kisha kujipatia shilingi Millioni 10.
Wakili Mafuru amedai kuwa shtaka la pili na la tatu linamkabili mtuhumiwa Barnaba Gidajuri aliyatenda Januari 4, 2024 akisambaza jumbe fupi kwa njia ya mtandao wenye maneno
“Mzee huyu Mganga wa tiba asili anatoa mali bila kafara, cheo, mapenzi…jiunge na chama huru cha freemason (666) Tanzania bila kutoa kafara ya binadamu…..”
Baada ya kusomewa mashtaka hayo washtakiwa hawakutakiwa kujibu kutokana na mahakama hiyo kutokuwa na mamlaka ya kusikiliza shauri hilo.
Washtakiwa wote wamerudishwa rumande kutokana na kesi yao kutokuwa na dhamana na kesi hiyo imeahirishwa
hadi June11, 2024.