Mkuu wa majeshi Namibia atembelea Tanzania

0
190

Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi ya Namibia, Air Marshal Martin Kambulu Pinehas na ujumbe wake amefanya ziara ya kikazi nchini kwa kutembelea Makao Makuu ya Jeshi Jijini Dar es Salaam na kukutana na mwenyeji wake, Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi, Jenerali Jacob Mkunda.

Air Marshal Penehas alipokelewa na kukagua gwaride rasmi la heshima lililoandaliwa kwa ajili yake katika Viwanja vya Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Upanga jijini Dar es Salaam.

Katika mazungumzo yao, Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi, Jenerali Mkunda amesema Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania Zanzibar (JWTZ) linafurahishwa kwa kuimarika kwa uhusiano wa kidiplomasia ya kijeshi baina ya Namibia na Tanzania.

Aidha, amesema kuwa ziara ya Mkuu wa Majeshi wa Namibia itaongeza chachu ya ushirikiano kati ya majeshi ya nchi hizo mbili hasa katika nyanja ya mafunzo ambapo majeshi haya yamekuwa yakishirikiana katika eneo hilo la mafunzo.

Mkuu wa Majeshi wa Namibia amesema amekuja Tanzania ili kujifunza kutokana na JWTZ kuwa mfano wa kuigwa katika ulinzi.

Aidha, Air Marshal Pinehas ameeleza kukumbuka juhudi za Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere za kuwawezesha Wanamibia kupata mafunzo ya kijeshi yaliyochangia kupatikana kwa uhuru wa kudumu wa nchi yao.

Amelipongeza JWTZ kwa kazi linayoifanya katika juhudi za kupatikana amani ya kudumu nchini Msumbiji ambapo Tanzania ina kikosi chake kinachoshiriki operesheni chini ya mwamvuli wa Jumuiya ya Maendeleo Nchi za Kusini mwa Afrika.