Watu zaidi ya 500 kutoka kaya 311 katika kijiji cha Manyara kata ya Magara wilayani Babati mkoani Manyara hawana makazi na chakula baada Ziwa Manyara kujaa maji na kusambaa katika makazi ya watu na mashamba, kufuatia mvua kubwa zinazoendelea kunyesha.
Mwenyekiti wa Kijiji cha Manyara, Juma Jorojik amesema mafuriko hayo yameathiri zaidi ya heka 200 za mpunga, mahindi, alizeti na mazao mengine ya chakula, huku kitongoji cha Kambi ya Fisi kikiathiriwa zaidi ambapo nyumba zaidi ya 100 zimezingirwa na maji.
Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Babati Vijijini Daniel Sillo ametembelea kijiji hicho na kutoa pole kwa wakazi ambao wameathiriwa na mafuriko hayo.
Pia amekabidhi msaada wa magunia 10 ya mahindi na kuwataka wananchi hao kuwa watulivu na kusaidiana wenyewe kwa wenyewe wakati Serikali ikiendelea na utaratibu mwingine.