Mazingira wezeshi na jumuishi ya kibiashara kuboreshwa

0
141

Asasi za Foundation For Civil Society (FCS) na TradeMark Africa zimesaini makubaliano ya utekelezaji wa mradi wa miaka mitatu wenye thamani ya shilingi bilioni 2.3 utakaoboresha mazingira wezeshi na jumuishi ya kibiashara nchini ili kuhakikisha wanawake, vijana na watu wenye ulemavu wanajumuishwa kikamilifu katika uendeshaji wa biashara, kukabiliana na changamoto za kimfumo katika biashara na mabadiliko ya tabianchi kama sehemu ya kuchochea ukuaji endelevu wa uchumi Tanzania.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi Mkazi wa Trademark Africa, Elibariki Shammy amesema mradi huo ni muhimu kutokana na kuwa na malengo ya kimkakati ya kuchochea ukuaji wa biashara ambao ni endelevu na shirikishi.

“Tunaamini kwamba kupitia ushirikiano huu wa kimkakati baina yetu na FCS, tunaweza kuleta matokeo chanya katika kuboresha mazingira ya biashara jumuishi nchini, kuwawezesha wanawake ni jambo la maendeleo, ukiwainua wanawake kibiashara unakuza uchumi na kuinua jamii nzima,” amesema Shammy.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa FCS, Justice Rutenge, amesema mradi huo utatoa elimu ya haki na ulinzi wa mlaji wa bidhaa mbalimbali nchini, ambayo ni changamoto kubwa kwa baadhi ya wananchi.

“Mradi huu ni muhimu katika kukuza soko la biashara la kitaifa na kimataifa, ushirikiano wetu na Trademark Africa ni hatua kubwa ya kulinda haki za mlaji nchini na kuweka mazingira bora na wezeshi ya kibiashara yanayokabiliana na changamoto za tabianchi,” amesema Rutenge.

Mradi huo wenye thamani ya dola za Marekani 900,000 umefadhiliwa na Ofisi ya Kigeni ya FCDO Uingereza, Ireland, na Norway, ukilenga kuunganisha nguvu za sekta binafsi na mashirika ya asasi za kiraia ili kuchochea ukuaji wa uchumi wa kijani.

📸✍️ @kingdee255 (David Mayunga)