Michezo ni afya na fursa ya ajira

0
329

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema michezo ni zaidi ya afya na burudani, ni fursa ya ajira na pia hupunguza magonjwa mwilini.

“Kama mnavyofahamu, michezo ni zaidi ya afya na burudani lakini leo tunathibitisha kuwa baada ya mbio hizi, sote tumefurahi na miili yetu imeimarika.”

Ametoa kauli hiyo leo Mei 11, 2024 wakati akizungumza na viongozi, wananchi na washiriki waliohudhuria hafla ya Tulia Marathon iliyofanyika kwenye Uwanja wa Sokoine, jijini Mbeya.

Amesema kwa mujibu wa Wizara ya Afya, michezo inawezesha watu kujikinga na magonjwa yasiyoambukiza. “Taarifa za Wizara zinasema kuwa nchi yetu inakabiliwa na changamoto ya ongezeko la magonjwa yasiyoambukiza kama vile shinikizo la damu, kisukari, kiharusi na maumivu ya viungo kama magoti na mgongo. Kwa hiyo tujenge tabia ya kufanya mazoezi, ” amesema.

Amesema hivi sasa fedha nyingi zinatumika kutibu maginjwa hayo iwe ni kwa Serikali au mtu mmoja mmoja na kwamba magonjwa hayo yanaendelea kupoteza nguvukazi ya Taifa.

Ametumia fursa hiyo kumpongeza Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa jitihada zake za kuboresha michezo na hivyo kuongeza hamasa ya kitaifa ya kupenda michezo.

“Sote tunakumbuka kuwa alianzisha mpango wa goli la mama, akaanzisha changizo la kitaifa kwa ajili ya timu za kitaifa na hii inaenda sambamba na michezo ijayo ya AFCON 2027.”