Aliyenasa kwenye jengo lililoporomoka Sauzi aokolewa

0
159

Wanandoa wameshiriki furaha yao na BBC baada ya kijana wao kuokolewa kutoka chini ya vifusi vya jengo lililoporomoka siku ya Jumatatu katika mji wa pwani wa Afrika Kusini wa George.

Delvin Safers anakuwa miongoni mwa watu 29 ambao wamethibitika kunusurika huku shughuli za uokoaji na utafutaji zikiendelea katika kuwatafuta watu wengine 39 ambao bado hawajulikani waliko.

Watu saba tayari wamethibitishwa kufariki dunia, na miili yao imeshaondolewa kwenye vifusi.

Delvin, 29, ambaye awali iliripotiwa kwamba ni mwanamke lakini ukweli ni mwanaume, aliwagusa wananchi wengi wa Afrika Kusini kwa jinsi alivyokuwa akiwatumia wazazi wake na mpenzi wake maelezo ya sauti ya kuhuzunisha moyo kupitia simu yake, akiwaambia jinsi anavyowapenda na kuelezea hofu kwamba hangeweza kutoka hai.

Baba yake, Dion Safers, ameiambia BBC kwamba yeye mwenyewe alikuwa na hofu kubwa hadi mtu mmoja alipompigia simu na kusema wamempata Delvin akiwa hai.

Hatua ya kupatikana kwake imeanzia kwa mbwa wa kunusa ambaye alianza kubweka, akiwatahadharisha waokoaji ambao walitoboa shimo kwenye zege eneo hilo hadi wakaweza kuona mkono wake.

“Walimpa chokoleti, maji, barakoa na miwani (ya kinga),” Dion ameongeza.

Mamake Delvin, Delmarie, ameiambia BBC kwamba mwanae alipokuwa amenasa chini ya vifusi, walimtumia picha ya mtoto wake wa miaka miwili, Zyar, ili kumtia moyo na na mtazamo chanya.

“Ilifanya kazi. Ilifanya kazi kweli,” amesema.

Katika moja ya maelezo yake ya sauti, kwa lugha ya Kiafrikana kwa mpenzi wake Nicole, Delvin alisema: “Mpenzi wangu, simu yangu ina chaji asilimia 5. Imezimwa. Nimeiwasha tu sasa ili kuiangalia.”

Pia alisikika akilia, na kusema: “Nina tumai timu za waokoaji zinaweza kufanya haraka kuniokoa kwa sababu hali yangu ni mbaya. Sina nguvu yoyote. Nimechoka, nimechoka, nimechoka…”

Jengo hilo la ghorofa tano liliporomoka lilipokuwa likijengwa katika jiji ambalo ni kivutio maarufu cha watalii, kando ya Barabara ya Garden Route, katika jimbo la Cape Magharibi.