Magari ya mizigo, mabasi na magari mengine madogo yaliyokwama kwa siku sita katika barabara ya Lindi – Dar es Salaam eneo la Njia Nne (Mikereng’ende hadi Somanga) yakitokea Lindi kuelekea Dar es Salaam yameruhusiwa kuendelea na safari.
Magari hayo yameruhisiwa kupita leo Mei 09, 2024 mara baada ya kukamilika kwa urejeshaji wa mawasiliano katika maeneo ya Mikereng’ende, Songas na Somanga ambayo yalikatika kutokana na mvua zilizonyesha na kuambatana na kimbunga Hidaya.
Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Zainab Telack amewataka wasafiri, wasafirishaji na watumiaji wengine wa barabara hiyo kusafiri kwa tahadhari kwa kuwa maeneo mengine yanaendelea na matengenezo.
“Naipongeza Serikali inayoongozwa na Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa jitihada zilizofanyika ndani ya muda mchache na leo tunashuhudia magari yaliyokwama yameruhusiwa kuendelea na safari”, amesema mkuu wa mkoa huyo wa Lindi
Aidha, kazi ya urejeshaji wa miundombini ya barabara ya Lindi – Dar es Salaam eneo la Nangurukuru ipo katika hatua ya ukamilishaji chini ya usimamizi wa Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa na timu ya wataalam kutoka
wizara hiyo na Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS).