Kamilisheni mchakato wa kupata ISO

0
275

Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mary Maganga ameupongeza Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF) kwa utoaji huduma unaofuata viwango vya Kimataifa katika kushughulikia masuala ya fidia kwa wafanyakazi.

Ameutaka mfuko huo kukamilisha mchakato wa kuipata Ithibati ya Viwango vya Kimataifa (ISO) ili kuendelea kutoa huduma bora na kuboresha utendaji, kwani huduma zinazotolewa tayari zimekidhi vigezo vya Shirika la Kimataifa la Viwango.

Maganga ameyasema hayo mkoani Dodoma alipotembelea ofisi za Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi, ikiwa ni sehemu ya ziara yake ya kutembelea taasisi zilizo chini ya
Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa WCF Dkt. John Mduma amemhakikishia Katibu Mkuu huyo kuwa watakamilisha mchakato wa kupata Ithibati ya ISO na kuongeza kuwa tayari wamepata Tuzo ya Kimataifa kwa utoaji huduma mtandao na Shirika la Kazi Duniani (ILO) limeutambua muongozo wa mfuko huo inaoutumia kufanya tathmini ya viwango vya ulemavu.