Maandamano makubwa yamefanyika katika maeneo mbalimbali nchini Australia, kupinga vitendo vinavyodaiwa kuwa ni vya unyanyasaji dhidi ya wanawake ambavyo vimeripotiwa katika siku za hivi karibuni.
Taarifa kutoka nchini Australia zinaeleza kuwa tangu mwaka huu uanze hadi sasa, wastani wa mwanamke mmoja huuawa kila baada ya siku nne, hali inayowafanya watu wengi nchini humo kuhisi kuwa huo ni unyanyasaji dhidi ya wanawake.
Katika tukio la karibuni kabisa mtu mmoja aliwachoma visu watu sita katika Kituo cha Biashara cha Sydney ambapo watano kati yao walikuwa ni wanawake, na hivyo kuchochea kufanyika kwa maandamano hayo.
Waandamanaji hao wametaka unyanyasaji dhidi ya wanawake ukomeshwe kwa Serikali kuchukua hatua kali kwa watu wote wanaofanya vitendo hivyo.