Mapande ya barafu yawa ghali Mali kuliko mkate

0
145

Joto kali ambalo limevunja rekodi limesababisha vipande vya barafu sasa kuuzwa kwa gharama kubwa kuliko mkate au paketi ndogo ya maziwa katika baadhi ya maeneo nchini Mali.

“Nimekuja kununua barafu kwa sababu kuna joto sana sasa,” anasema Fatouma Yattara, binti mwenye umri wa miaka 15 akiwa amesimama nje ya duka katika mji mkuu wa mali, Bamako.

Huku friji likiwa halifanyi kazi kwa sababu ya kukatika kwa umeme kwa muda mrefu nyumbani kwao (na maeneo mengi ya nchi), Fatouma anasema familia imeamua kutumia mabarafu ili kuhifadhi chakula na kuweka kwenye maji ya kunywa yapate baridi wakati huu ambao joto nchini humo limepanda hadi kufikia nyuzijoto 48C.

Kumbuka kwa Tanzania, taarifa ya joto iliyotolewa na Mamlaka ya Hali Hewa Januari 3 mwaka huu ilisema kwamba hadi kufikia Desemba 29, 2023 kituo cha Morogoro ndicho kiliripoti kiwango cha juu zaidi cha nyuzi joto cha 33.9C

Binti huyo mdogo anasema kupanda kwa bei ya barafu kunafanya maisha kuwa magumu. “Katika baadhi ya maeneo ni kati ya faranga 200 hadi 500 (zaidi ya shilingi 1,000) kwa mfuko mdogo. Ni ghali sana,” anasema.

Hii inafanya barafu kuwa ghali zaidi kuliko mkate ambao kwa kawaida huuzwa wastani wa Faranga 250.

Chanzo: BBC