Mafuriko yachelewesha shule kufunguliwa Kenya

0
269

Serikali ya Kenya imeahirisha kufunguliwa kwa shule kwa wiki moja zaidi kutokana na mafuriko ambayo yamesababisha vifo vya zaidi ya watu 80 kufikia sasa.

Takwimu zinaonesha kwamba shule nyingi nchini humo zimeathiriwa vibaya na mafuriko, Waziri wa Elimu wa Kenya, Ezekiel Machogu amesema katika taarifa yake iliyotolewa jana Jumapili.

“Athari za mvua katika baadhi ya shule ni kubwa kiasi kwamba haitakuwa jambo la busara kuhatarisha maisha ya wanafunzi na wafanyakazi kwa kuruhusu shule kuwa wazi katika mazingira ya sasa,” ameongeza waziri.

Shule zote, ambazo zilitakiwa kufunguliwa kwa muhula wa pili Aprili 29, sasa zitafunguliwa Mei 6.

Baadhi ya shule pia zinatumika kuhifadhi watu ambao wamehamishwa kutoka maeneo yaliyokumbwa na mafuriko.

Kufikia Jumamosi, idadi iliyothibitishwa ya waliofariki dunia kutokana na mafuriko iliongezeka hadi 83 baada ya miili 13 zaidi kupatikana katika maeneo tofauti ya nchi. Huenda idadi ya vifo ikaongezeka kutokana na mvua zianazoendelea kunyesha nchini Kenya.

Zaidi ya watu 130,000 wamehama makazi yao kutokana na mafuriko hayo, mamlaka ilisema, huku makumi ya watu wakiripotiwa kupotea.

Kenya na mataifa mengine ya Afrika Mashariki yameathiriwa na mafuriko katika wiki za hivi karibuni.