21 wabambwa na kilo 767 dawa za kulevya

0
152

Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA), imekamata kilo 767.2 za dawa za kulevya kupitia operesheni zilizofanyika katika mikoa ya Dares Salaam, Pwani na Tanga kuanzia Aprili 4 hadi 18, 2024.

Kamishna Jenerali wa DCEA, Aretas Lyimo amesema, kati ya dawa zilizokamatwa, heroin ni kilo 233.2, methamphetamine kilo 525.67 na skanka kilo 8.33.

Amesema katika operesheni hiyo watuhumiwa 21 wamekamatwa kuhusika na dawa hizo na kwamba baadhi yao wamefikishwa mahakamani na wengine watafikishwa pindi taratibu za kisheria zitakapokamilika.

Aretas amebainisha kuwa biashara na matumizi ya dawa za kulevya ni moja ya matishio makubwa ya kiusalama duniani hasa ikizingatiwa kuwa, vijana ndio kundi linaloathiriwa zaidi na dawa hizo.

Amesema kwa mujibu wa takwimu ya sensa ya watu na makazi ya mwaka 2022, idadi ya vijana ambao ndio nguvu kazi ya Taifa ni takribani milioni 20 sawa na wastani wa asilimia 50 ya Watanzania wote.

Lymo ameongeza kuwa idadi kubwa ya watuhumiwa waliokamatwa ni vijana na kwamba endapo kundi hili litaendelea kujiingiza kwenye biashara na matumizi ya dawa za kulevya litapoteza ustawi binafsi na taifa litapoteza nguvu kazi muhimu