Makamu wa Rais, Dkt. Philip Mpango ameagiza Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi pamoja na mamlaka za miji, halmashauri na majiji kuchukua hatua za makusudi kulinda maeneo yote yaliyotengwa kwa ajili ya “bustani za kijani” na kuhakikisha hayavamiwi au kubadilishwa matumizi.
Makamu wa Rais ametoa maagizo hayo wakati akifungua Kongamano la Kuhamasisha Uwekezaji katika Bustani za Kijani nchini kwa Maendeleo Endelevu (Green Parks) lililoandaliwa na Jukwaa la Maendeleo endelevu linalofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa St. Gaspar mkoani Dodoma.
Ametaka maeneo hayo kupimwa na kuwekewa alama za kudumu kuonesha mipaka yake pamoja na kuagiza mamlaka za serikali za mitaa kutunga sheria ndogo (by-laws) na kusimamia utekelezaji wake ili kuhakikisha maeneo ya bustani za kijani yanalindwa na kutumika kama ilivyokusudiwa.
Aidha Makamu wa Rais ametoa wito kwa sekta binafsi, mashirika, taasisi za umma pamoja na taasisi za dini kuwekeza katika uanzishaji na uendelezaji wa bustani za kijani nchini kwa maendeleo endelevu.
Pia amesema makampuni binafsi na mashirika ya umma yanapaswa kujumuishwa na kushiriki katika uanzishaji, utunzaji na uendelezaji wa bustani za kijani kuwa sehemu ya wajibu wao wa kurejesha faida kwa jamii (CSR).
Ametoa wito kwa mamlaka zote za miji, halmashauri za wilaya na majiji kushindanisha vijana wa Kitanzania kubuni bustani bora za kijani katika makao makuu ya wilaya, mikoa, miji au majiji.