Watumiaji barabara ya Moshi – Arusha wakwama

0
324

Mamia ya watumiaji wa barabara ya Moshi Arusha wamekwama kwa saa kadhaa katika eneo la Kwa Msomali kufuatia Mto Sanya kujaa maji kutokana na mvua zinazoendelea kunyesha wilayani Hai mkoani Kilimanjaro.

Akizungumzia hali hiyo, Meneja wa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) mkoa wa Kilimanjaro Mhandisi Motta Kyando amesema chanzo cha hali hiyo ni maji kujaa pamoja na kuwepo kwa magogo juu ya daraja hilo na hivyo kusababisha magari kushindwa kupita.

Mhandisi Kyando amesema kwa sasa wanaendelea na taratibu za kuondoa magogo, kusafisha eneo hilo na kuimarisha tuta la barabara ili kuhakikisha barabara inapitika bila usumbufu wowote.

Amebainisha kuwa daraja lililopata changamoto hiyo ni la Sanya na sio daraja la Mto Biriri ambalo limejengwa hivi karibuni.

Tayari magari yameruhusiwa kupita katika daraja la Sanya kwa upande mmoja wa barabara.