Mamelodi wamwinda Aziz Ki, mwenyewe afunguka

0
2925

Miamba ya soka ya Afrika Kusini, Mamelodi Sundowns wanahusishwa kuiwinda saini ya kiungo wa Yanga SC na raia wa Burkina Faso, Stephane Aziz Ki.

Masandawana wanaonekana kuvutiwa na kiwango cha Ki, hasa katika michezo ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika ambapo aliitikisa ngome yao ya ulinzi.

Baada ya mchezo wa duru ya pili kati ya timu hizi, Kocha wa Masandawana alikwenda alipokuwa ameketi Aziz Ki na kumnyanyua kisha kumfariji baada ya Yanga kutolewa katika mazingira ambayo yanasemekana kutokuwa halali, kitendo ambacho hakikumfurahisha kocha msaidizi wa Yanga, na kupelekea mvutano uwanjani hapo.

Hata hivyo kupitia ukurasa wake wa Instagram, Aziz Ki amewaambia mashabiki wa Yanga kwamba hana mpango wa kuondoka Jangwani, kwani kilichomleta kwenye timu hiyo bado hajakifanikisha.

“Hata pesa hauwezi kufikia kiwango cha upendo nilio nao kwa klabu hii (Yanga),” ameandika kupitia ukurasa wake wa Instagram akisistiza kwamba kilichomleta ni kutwaa mataji ya kimataifa na bado hajafanikiwa.

“Nina deni kubwa kwenu (mashabiki wa Yanga) na Yanga ni familia yangu,” ameeleza zaidi baada ya shabiki mmoja kumuuliza kama ni kweli anaondoka.