Tanzania imepitia mabadiliko makubwa kwenye sekta ya fedha yakichochewa na kasi ya ongezeko la matumizi ya teknolojia katika kuzalisha na kusambaza bidhaa na huduma za kifedha.
Pamoja na hayo yanayoifanya Tanzania kubaki kuwa mstari wa mbele katika masuala ya huduma jumuishi za kifedha, bado upo uwiano usio sawa katika upatikanaji na matumizi ya huduma rasmi za kifedha nchi nzima kwa rika la watu wa wazima.
Kwa mujibu wa matokeo ya utafiti wa FinScope 2023, kiwango cha upatikanaji na matumizi ya huduma rasmi za kifedha kiliongezeka hadi kufikia asilimia 89 na asilimia 76 mwaka 2023 kutoka asilimia 86 na asilimia 65 mwaka 2017, mtawalia.
Hata hivyo, kiwango cha watu walio nje ya huduma rasmi za kifedha bado kipo juu kwa baadhi ya makundi yakiwemo ya Watanzania wanaoshi vijijini, wakulima wadogo, vijana na wanawake.